Slide1-1-465x364

Majaribio ya chanjo ya ChAdOx1 nCoV-19: Maswali yanayoulizwa mara kwa mara

1. Je majaribio ya chanjo ya ChAdOx1 nCOV-19 ni nini? Majaribio haya yanalenga kutathmini ikiwa chanjo ya ChAdOx1 nCOV-19 ni salama, inafanya kazi na inapeana kinga dhidi ya COVID-19 kwa watu wazima wenye umri wa miaka 18 na zaidi

2. Majaribio ya chanjo hii yatachukuwa muda gani? Baada ya kuanza, majaribio yatafanyika kwa muda wa miezi 24.

3. Kwa nini tufanye majaribio haya hapa nchini Kenya? Chanjo inayofanya kazi katika jamii moja sio kwamba itafanya kazi katika jamii zote, kwa hivyo, ni muhimu kujua ikiwa chanjo hii ya majaribio inafanya kazi katika jamii za Kenya kuhakikisha kwamba waKenya wanaweza kunufaika na chanjo hiyo iwapo itaonekana kuwa na ufanisi.

4. Je Kenya itanufaika vipi kwa kushiriki kwenye majaribio haya ya chanjo? Tunahitaji kujua ikiwa chanjo hii inafanya kazi katika jamii yetu, ili serikali ya Kenya iamue ikiwa itawekeza kwenye chanjo hii au la. Serikali ya Kenya, kupitia wizara ya afya itaweza kuanzisha majadiliano na watengenezaji wa chanjo na wafadhili, kujua njia za kufanya chanjo hii kufikiwa/kupatikana na wakenya kwa gharama ya chini. Duniani kote, kuna majadiliano kati ya mashirika ya duniani kote ya mipango ya chanjo kama vile GAVI (Muungano wa chanjo) na serikali za nchi kadhaa, ili kufikia makubaliano ya jinsi chanjo zinazofanya kazi zitasambazwa miongoni mwa wananchi.

5Majaribio haya yatafanyika wapi? Kituo cha kwanza cha usajili kitakuwa Kilifi na usajili nje ya kaunti ya Kilifi utakuwa kulingana na janga litakavyokuwa linaendelea na unaweza kujumuisha Mombasa.

6Kwa nini majaribio haya yanafanyika Kilifi? Ufuatilizi unaofaa ni muhimu sana katika majaribio ya awamu ya 1 na ya 2, na ufuatilizi huu unafanyika kwa urahisi katika maeneo yaliyo na mfumo wa ufuatilizi wa idadi ya watu.

7. Ni watu wangapi watakaosajiliwa kwenye majaribio haya? Jumla ya watu wazima 400 waliojitolea watasajiliwa kwa awamu ya 1b na ya 2.

8. Ni nani anayeweza kushiriki kwenye majaribio haya? Majaribio haya yatajumuisha watu ambao kazi zao zinawalazimu kutangamana na watu mara kwa mara katika maeneo yanayotoa huduma muhimu kama vile wahudumu wa afya, madereva wa magari ya mizigo, wafanyikazi wa mambo ya usalama miongoni mwa watu wengine, wenye umri wa zaidi ya miaka 18

9. Je awamu za majaribio ya chanjo hii ni zipi? Utafiti huu unahusisha awamu mbili. Katika awamu ya kwanza, washiriki 40 watasajiliwa; na kufuatwa na washiriki 360 watakaosajiliwa katika awamu ya pili ya utafiti huu.

10. Je chanjo hii ni salama? Athari inayoweza kutokea kwa washiriki iko chini sana, na hasa inahusiana na kuchukua kwa sampuli ya damu na kudungwa chanjo.

11. Je chanjo hii ni salama? Chanjo hii ya majaribio kufikia sasa imepeanwa kwa washiriki zaidi ya 8,000 huko Uingereza, Afrika Kusini na Brazil, na hakuna wasiwasi mkubwa wa usalama ulioonekana.

12. Majaribio ya chanjo hii yalisitishwa katika nchi nyengine, kwa nini mwaijaribu hapa Kenya? Majaribio yalisitishwa kwa muda mfupi wakati mshiriki mmoja alipata ugonjwa usiotarajiwa. Kusitishwa kwa majaribio ni utaratibu wa kawaida unaoruhusu kundi la watu huru kufanya uchunguzi wa kilichosababisha ugonjwa fulani ambao umetokea kwa mshiriki wa majaribio. Wakati majaribio yalipositishwa, usajili wa washiriki haukuwa unaendelea hapa Kenya.

13. Je majaribio ya chanjo hii yamesitishwa kabisa? Kufuatia ukaguzi ulio huru wa kilichosababisha ugonjwa wa mshiriki wa majaribio haya, na kutambua kwamba inawezekana haikuhuisana na chanjo ya majaribio, bodi ya kufuatilia habari za usalama [Data Safety and Monitoring Board (DSMB)], imeruhusu majaribio yaendelee.

14. DSMB ni nini? Hii ni kamati huru ya wataalam wa maswala ya utafiti wa kimatibabu. Wanakamati ni wa kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kazi yao ni kufuatilia kwa ukaribu habari za usalama zinazotoka kwa majaribio ya dawa/chanjo. DSMB ya majaribio ya chanjo hii inajumuisha wanasayansi wenye utaalam kutoka Kenya. Mamlaka zinazoidhinisha za Kenya zinaendelea kupewa habari punde zinapotokea zinazohusu mambo yote ya usalama katika majaribio ya kimataifa.

15. Mtahakikisha vipi usalama wa washiriki? Washiriki watafuatiliwa kwa ukaribu wakati wa majaribio haya kuhakikisha wako na afya nzuri, na madhara yoyote ya chanjo hii yanashuhulikiwa. Watafuatiliwa kwa muda usiozidi miezi 12 baada ya kupata chanjo ya majaribio.

16. Je watu wanalipwa kwa kushiriki kwenye majaribio haya? Watu watakaokubali kujitolea kushiriki kwenye majaribio haya wataregeshewa gharama zao za kushiriki kama vile tikiti. Pia watapewa fidia ya gharama nyengine zinazohusiana na utafiti ambazo wanaweza kuzipata, kwa kiwango maalum kama kilivyowekwa kwenye muongozo wetu wa malipo. Kulipa gharama za washiriki ni jambo la kimaadili linalohitajika katika utafiti.

17. Je manufaa yanayoweza kupatikana kwa wanaoshiriki ni gani? Washiriki watanufaika na ufahamu wa hali yao ya afya kwa jumla, ikijumuisha ikiwa wameambukizwa na SARS-CoV-2 (kirusi kinachosababisha COVID-19)

18. Je washiriki watafikia/watapata chanjo hii bila malipo iwapo itaonekana inafanya kazi? Iwapo habari/data kote ulimwenguni zitaonyesha usalama na utendajikazi wa chanjo hii ya majaribio, kundi la kudhibiti litakalopokea chanjo ya kichaa cha mbwa litapewa chanjo ya ChAdOx1 nCoV-19, mara tu muongozo unaofaa utakapokuwa umefuatiliwa.

19. Ni nani aliyetengeneza chanjo hii? Chanjo hii imetengenezwa na watafiti kutika chuo kikuu cha Oxford, Uingereza, wakishirikiana na AstraZeneca.

20. Je majibu ya majaribio haya yatasambazwa vipi kwa wananchi? Habari kwa muhtasari za matokeo ya majaribio zitapeanwa katika mikutano ya wanajamii katika maeneo ambayo washiriki walisajiliwa. Pia, habari kwa washikadau wote zitapeanwa kupitia njia mwafaka za mawasiliano na za ujumuishaji wa watu.

21. Je KWTRP iko na uwezo gani wa kufanya majaribio haya? Watafiti wa KWTRP wamefanya majaribio makubwa ya chanjo ndani ya muda wa miaka zaidi ya ishirini kama vile majaribio ya chanjo ya malaria ya RTSS na majaribio ya chanjo ya Ebola.

22. Ni nani anayefadhili majaribio haya? Majaribio haya yamefadhiliwa na Wellcome Trust na chuo kikuu cha Oxford.

23. Je tutarajie majibu ya majaribio haya lini? Tayari tuko na habari nyingi kuhusu usalama na ubora wa utendajikazi wa chanjo hii, hatuwezi kujua ni lini tutakapoweza kuamua ikiwa chanjo inakinga ugonjwa. Hii itategemea janga, pale wagonjwa wanapopungua, ni vigumu kujua ikiwa chanjo inakinga ugonjwa.